Dunia

sayari ya tatu kutoka kwenye Jua katika Mfumo wa Jua
(Elekezwa kutoka Duniani)

Dunia ni kiolwa cha angani ambapo juu yake tunaishi sisi binadamu na viumbehai wengine wengi, tukipata mahitaji yetu, kuanzia hewa ya kutufaa na maji.

Dunia
Dunia katika anga-nje, kama ilivyoonwa na wanaanga wa Apollo 17.
Dunia katika anga-nje, kama ilivyoonwa na wanaanga wa Apollo 17.
Jina
Asili ya jinaKar. دنيا, (dunyaa)
Majina mengine
Ardhi, nchi
Alama🜨
Tabia za mzunguko
Mkaribiokm 147,098,450
au 0.983292
Upeokm 152,097,597
au 1.01671
km 149,598,023
au 1.0
Uduaradufu0.0167086
siku 365.256363004
Mwinamo0.00005° toka njia ya Jua
MieziMwezi
Tabia za maumbile
km 6371.0
Tungamokg 5.972168×1024
g/cm3 5.5134
Uvutano wa usoni
m/s2 9.80665
siku 1.0
siku 0.99726968
Weupe0.306 (Bond)
0.367 (jiometri)
HalijotoK 287.91 (14.76°C)

Dunia ni mojawapo ya sayari nane zinazozunguka Jua letu katika anga-nje. Kati ya sayari za Mfumo wa Jua, Dunia yetu ni sayari ya tatu kutoka kwa Jua.

Masafa baina yake na Jua ni kilomita milioni 150 au kizio astronomia 1. Dunia huchukua siku 365.256 kulizunguka Jua, na masaa 23.9345 kuuzunguka mhimili wake na upana wake ni kilomita 12,756.

Umri wa Dunia hukadiriwa kuwa miaka bilioni 4.5[1][2].

Ni mahali pekee katika ulimwengu panapojulikana kuna uhai ulioaminiwa kuanza miaka bilioni 3.5 iliyopita[3].

Uhai unapatikana kwa spishi milioni 10-14 za viumbe hai pamoja na wanadamu waliokadiriwa kuwa sasa bilioni 7.2[4].

Umbo la Dunia

Umbo la Dunia linafanana na tufe au mpira unaozunguka kwenye mhimili wake. "Mhimili wa Dunia" ni mstari kati ya ncha zake.

Lakini si tufe kamili. Ina uvimbe kidogo kwenye sehemu ya ikweta; ilhali umbali kati ya ncha mbili ni kilomita 12,713 lakini umbali kati ya sehemu za kinyume kwenye ikweta ni km 12,756, yaani kipenyo hiki kinazidi takriban kilomita 43 kipenyo kati ya ncha na ncha. Tofauti hii inasababishwa na mzunguko wa Dunia. Kani nje inasukuma sehemu za ikweta nje zaidi. Kwa hiyo mahali Duniani palipo karibu zaidi na anga-nje si Mlima Everest kwenye Himalaya bali mlima Chimborazo nchini Ekuador.[5]

Kwenye uso wake Dunia huwa na tofauti kati ya nusutufe zake mbili. Nusu moja ina eneo kubwa la mabara yaani nchi kavu ambayo ni asilimia 47 ya sehemu hii. Kinyume nusutufe nyingine inafunikwa na maji ya bahari na eneo la nchi kavu ni asilimia 11 pekee za maeneo yake.

Kwa jumla Dunia ni sayari pekee katika Mfumo wa Jua yenye maji katika hali ya kiowevu usoni mwake. Bahari kuu ya Dunia inashika asilimia 96.5 ya maji yote yaliyopo Duniani. Maji ya bahari huwa na asilimia 3.5 chumvi ndani yake.

Kwa pamoja maeneo ya maji hufunika 70.7% za uso wa Dunia. Nchi kavu huwa na 29.3% na sehemu kubwa ya eneo la nchi kavu ni bara 7 za Asia, Afrika, Amerika Kaskazini, Amerika Kusini, Antarktika, Ulaya na Australia. (Ulaya inaweza kuangaliwa pia kama sehemu ya Asia ikiwa kama rasi yake ya magharibi. Azimio la kutazama Australia kama bara na Greenland kama kisiwa tu ni azimio la hiari si la lazima).

 
Dunia jinsi inavyozunguka kwenye mstari wa mhimili wake

Maeneo ya bahari kuu ya Dunia kwa kawaida hugawiwa kwa bahari kubwa 3 za Pasifiki, Atlantiki na Bahari ya Hindi. Sehemu ya chini baharini iko kwenye Mfereji wa Mariana katika Pasifiki (mita 11,034 chini ya UB). Kwa wastani bahari huwa na kina cha mita 3,800.

Muundo wa Dunia

- taz. makala "Muundo wa Dunia" -
 
Nusutufe ya Dunia yenye maji mengi
 
Matabaka yaliyopo katika muundo wa Dunia.

Tumeona Dunia ina umbo la mviringo au tufe. Tufe hilo si kipande kimoja kikubwa cha mwamba thabiti. Dunia ina muundo ndani yake. Muundo huo unafanana kiasi na kitunguu, yaani Dunia yetu imefanyika kwa matabaka mbalimbali yanayofuatana kutoka nje kwenda ndani. Kila moja lina tabia yake.

Kimsingi wataalamu hutofautisha matabaka matatu ambayo ni:

Ganda la Dunia ni sehemu imara na uhai wote tunaouJua unapatikana juu yake. Katikati hali ya koti na ya kiini ni ya joto kubwa sana na maada yake hupatikana katika hali ya giligili (si imara, kuyeyushwa). Kila ukiingia ndani Dunia inazidi kuwa ya moto mpaka ukifika ndani kabisa daraja ya harara hufikia nyuzi 5000-6000 °C.

Matabaka hayo yanafanywa kwa elementi za kikemia ambazo ni feri (chuma) (32.1%), oksijeni (30.1%), silisi (15.1%), magnesi (13.9%), sulfuri (2.9%), nikeli (1.8%), kalsi (1.5%) na alumini (1.4%). Mabaki ya 1.2% ni viwango vidogo vya elementi nyingine. Elementi hizo zinapatikana kwa hali safi au katika kampaundi za elementi.

Vipimo vimeonyesha ya kwamba matabaka mawili ya koti na kiini huwa tena na mgawanyiko ndani yake, hivyo matabaka yafuatayo yanaweza kutofautishwa.

Tabaka Kuanzia kilomita
Ganda la nje 0 - 40
Koti la juu 40 - 400
Koti la kati 400 - 900
Koti la chini 650 - 2900
Kiini cha nje 2900 - 5100
Kiini cha ndani 5100-6371

Sehemu ya juu ya koti inafanana kikemia na ganda na sehemu hizo mbili zinaitwa tabakamwamba. Tabakamwamba ina unene wa kilomita 50 - 100.

Tabakamwamba imekatika katika vipande vinavyoitwa mabamba la ganDunia. Vipande hivi vinaelea juu ya giligili ya koti la ndani. Ndiyo sababu bara lolote si la milele; kila bamba huwa na mwendo wake na ndiyo sababu katika historia ya Dunia mabara yameachana na kuungana mara kadhaa. Kwa mfano imepimwa ya kwamba sehemu kubwa ya Afrika ya Mashariki ina mwendo wa kuachana na bara la Afrika na dalili yake ni bonde la ufa.

Pale ambako mabamba yanapakana, volkeno nyingi zinapatikana na matetemeko ya ardhi hutokea.

Ugasumaku wa Dunia

 
Mnururisho unavyotoka kwenye Jua na kukengeushwa na mistari ya nguvu ya sumaku ya ugasumaku wa Dunia

Dunia inazungukwa na uga sumaku yaani mistari ya nguvu ya kisumaku. Sababu yake ni kwamba kiini cha Dunia kinafanywa na chuma chenye tabia kama sumaku kubwa.

Tabia hiyo inasababishwa na mwendo wa mikondo ya chuma cha moto kilichoyeyuka katika kiini cha nje cha Dunia. Mistari ya nguvu ya sumaku inatoka nje kwenye ncha ya kusini na kurudi ndani ya Dunia kwenye ncha ya kaskazini. Tabia hiyo ni msingi wa kazi ya dira ambamo sindano ya dira huvutwa daima na ncha sumaku ya Dunia na kuelekea kaskazini muda wote.

Ugasumaku wa Dunia ni kinga muhimu kwa uhai wote Duniani. Dunia inapigwa muda wote na mnururisho kutoka Jua kwa njia ya "upepo wa Jua". Mnururisho huo ni nuru pamoja miale ya hatari. Ugasumaku unakengeusha sehemu kubwa ya mnururisho hatari hadi unapita kando ya Dunia na kutofika kwenye uso wa Dunia.

Dunia kama mahali pa uhai

Dunia yetu ni sayari pekee inayojulikana mpaka sasa ambapo binadamu na viumbe vingine vinaweza kuishi. Wanasayansi bado wanafanya ufafiti kuJua kama kuna kuna viumbe hai kwenye sayari nyingine.

Hapa kuna sababu mbili zinazofanya viumbehai kuishi Dunianiː

  1. Dunia yetu ina umbali na Jua unaofaa kwa maisha kwa sababu sayari zilizoko karibu zaidi na Jua (k.m. Zuhura) zina joto kubwa mno na sayari zilizoko mbali zaidi kama Mrihi ni baridi mno.
  2. Dunia yetu ina angahewa yenye asilimia 78 ya naitrojini, asilimia 21 ya oksijini na asilimia 1 ya aina nyinginezo za hewa, na kwa sababu hii uhai na maisha yanamakinika katika ardhi, kinyume na sayari nyinginezo.

Uso wa Dunia

 
Picha ya Dunia ikionyesha kutokea kwa mabara kutoka kugawanyika kwa Pangea mpaka hivi leo.

Sehemu kubwa kabisa ya Dunia inafunikwa na bahari, kwani takriban asilimia 70 ya uso wake unafunikwa na maji ya bahari na kutokana na maji yote yaliyokuwepo ardhini, asilimia 97 ni maji ya bahari, na asilimia 3 ni maji matamu. Theluthi inayobaki ni nchi kavu kwenye mabara mbalimali na visiwa vingi.

Sura ya Dunia ni kilomita mraba 510,000,000, ikiwa nchi kavu imechukua eneo la kilomita mraba 149,430,000 na maji yamechukua eneo la kilomita mraba 360,570,000.

Bahari Kuu Eneo lake (kilomita za mraba) Asilimia
Pasifiki 168,723,000 46.6
Atlantiki 85,133,000 23.5
Bahari Hindi 70,560,000 19.5
Bahari ya Antaktiki 21,960,000 6.1
Bahari ya Aktiki 15,558,000 4.3

Mabara makubwa ni Asia, Afrika, Amerika Kusini na Amerika Kaskazini, Australia na Ulaya. Asia na Ulaya mara nyingi hutazamiwa wakati mwingine kama bara moja ya Eurasia.

Angahewa

Hewa iliyoko juu ya ardhi vile vile ina matabaka mbalimbali, na kila tabaka lina kazi yake. Hewa kwa jumla ina masafa ya kiasi cha kilomita 560 au maili 348 kuendea juu, na baada ya hapo unaingia kwenye anga-nje. Hewa hiyo ndiyo inayokinga viumbehai na madhara ya Jua na mnururisho wa angani ambao unaingia anga ya Dunia na kuteremka chini.

Tazama pia

Marejeo

  1. G. Brent Dalrymple: The age of the Earth in the twentieth century: a problem (mostly) solved, The Geological Society of London 2001
  2. Chris Stassen, The Age of the Earth, (The Talk Origins Archive, 2005)
  3. Schopf, JW, Kudryavtsev, AB, Czaja, AD, and Tripathi, AB. (2007). Evidence of Archean life: Stromatolites and microfossils. Precambrian Research 158:141–155.
  4. http://www.worldometers.info/world-population/
  5. Robert Krulwitch, The 'Highest' Spot on Earth? Mlima Everest ni mlima mrefu duniani wenye kimo cha juu ya uwiano wa bahari; lakini Chimborazo (mita 6,268 juu ya UB) iko karibu na ikweta, hivyo msingi wake uko juu ya uvimbe wa ikweta, kwa hiyo ni mahali ambako ni mbali zaidi na kitovu cha dunia na karibu zaidi na mwezi!
  • Cesare Emilliani: Planet Earth. Cosmology, Geology, and the Evolution of Live and Environment. Cambridge University Press 1992, ISBN 0-521-40949-7
  • Comins, Neil F. (2001). Discovering the Essential Universe (2nd ed.). W. H. Freeman. Bibcode:2003deu..book.....C. ISBN 0-7167-5804-0.

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dunia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.