Nenda kwa yaliyomo

Iramba

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 13:34, 5 Aprili 2024 na Riccardo Riccioni (majadiliano | michango)
(tofauti) ← Pitio lililotangulia | Toleo la sasa (tofauti) | Pitio linalofuata → (tofauti)
Mahali pa Iramba (kijani cheusi) katika mkoa wa Singida.

Wilaya ya Iramba ni wilaya mojawapo kati ya 7 za Mkoa wa Singida.

Imepakana na Mkoa wa Shinyanga upande wa kaskazini-Magharibi, na Mkoa wa Mara upande wa kaskazini-mashariki, wilaya ya Singida Vijijini na Singida Mjini upande wa kusini na Mkoa wa Tabora upande wa magharibi

Katika sensa ya mwaka 2022 walihesabiwa 328,912 [1]. Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 236,282.[2]

Sehemu kubwa ya wenyeji wa Iramba ni Wanyiramba wanaosema lugha ya Kinyiramba.

Kuanzishwa kwa Wilaya ya Iramba

[hariri | hariri chanzo]

Wilaya ya Iramba ilianzishwa mwaka 1954; awali makao makuu ya wilaya yalipelekwa kijiji cha Mkalama: huko hayakudumu kwani yalihamishiwa katika kijiji cha Kisiriri, hata hivyo watawala walipendezwa zaidi na eneo la Kiomboi ambalo lilikuwa na miti mingi aina ya miombo ambayo kwa Kinyiramba huitwa “mupumpu”. Wazungu walishindwa kutamka neno miombo na badala yake wakawa wanatamka kiomboi; neno hili lilipata mashiko kwa watumiaji kiasi cha kukomaa na kuwa Kiomboi.

Wilaya ya Iramba imeongozwa na wakuu wa wilaya mbalimbali kama ifuatavyo: 1. Dunstan A.Omari- 1958-Juni 1959, 2. Athuman Katuo -Julai 1959-Novemba 1960, 3. John M.Ndingwangu- Des. 1960-Juni 1961, 4. Samwel A.Msindai- Julai 1961- Nov 1962, 5. Sumbu Gallawa- Des.1962-Jan.1963, 6. G.M.Bundalla Feb.1963-Mei.1966, 7. G.O.Mhagama - Juni.1966-Machi,1967, 8. A.K.Msonge A pril.1967-Des.1971, 9. M.B.Kig’ombe Jan.1972-April 1977, 10. R.S.Chazua Julai 1977-Juni.1983, 11. Jeremia E.Duwe Julai 1983-Mei 1986, 12. A.K.Mwakyusa Mei 1986-Nov.1990, 13. E.M.Halinga Des.1990-Mei 1992, 14. John Z.Chiligati- Juni 1992-Des.1996, 15. David W.Hollela- Jani 1997-Aprili 1998, 16. Zainabu M.Kondo Aprili 1998-Agosti 2006, 17. Grace H.Mesaki Agosti 2006-Mei 2012, 18. Yahya E.Nawanda Mei 2012-Machi 2015, 19. Lucy Mayenga Machi.2015-Julai 2016, 20. Emmanuel J.Luhahula Julai.2016

Kuanzishwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba

[hariri | hariri chanzo]

Halmashauri ya Wilaya ya Iramba ilianzishwa mwaka 1984. Wakurugenzi watendaji wa halmashauri ya wilaya walioongoza wilaya hii ni hawa wafuatao: 1. George Challe-1984-1985, 2. Masanga B.Msonge-1985-1988, 3. Kabeja B.Moses-1988-1990, 4. Fredrick kipigapasi-1990-1995, 5. Berther Swai-1995-1997, 6. Mr.Msoma-1997-1998, 7. Ester Mbigili-1998-2000, 8. Mpangalukela Tatala-2000-2004, 9. Dr.Izidor Mtalo-2004-2007, 10.Fortunatus Fwema-2007-2012, 11.Christine K.Midello-2012-2013,12.Halima Mpita-2013-2015, 13.Dr.Grace Mbaruku-2015-2015, 14.Clement Berege-2015-2016, 15.Linno P.Mwageni-2016-Siasa

Wilaya ya Iramba imeweza kushiriki kikamilifu katika masuala ya siasa, hii ni pamoja na kufanya chaguzi mbalimbali kuwapata viongozi kuanzia ngazi ya shina hadi taifa 1958-1965 – Samwel Msindai 1965-1970 – Yona J. Nkurlu 1970-1975 Jimbo la Iramba liligawanywa kuwa majimbo mawili yaani Iramba ya juu na Iramba ya chini, ambapo Iramba ya juu alichaguliwa Mchungaji Simion P. Kinzu na Iramba ya chini alichaguliwa Ndg Abel Naligingwa. 1975-1980- Likarudishwa jimbo moja la Iramba lililoongozwa na Nassania Y. Nkurlu 1980-1995- Alichaguliwa Mhe, Nalaila L. Kiula 1995- Jimbo la Iramba liligawanywa majimbo mawili, jimbo la Iramba Magharibi na Iramba Mashariki, Nalaila Kiula aliongoza jimbo la Iramba magharibi na Mgana Msindai aliongoza Iramba Mashariki. 1995-2000- Nalaila Kiula (Iramba Magharibi). 2000-2005- Leonard Shango (Iramba Magharibi) 2005-2010- Juma Kilimba (Iramba Magharibi) 2010-2015- Mwigulu L. Nchemba (Iramba Magharibi) 2015- Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Mhe Diana Mkumbo Chilolo na Martha Mlata ni wabunge waliochaguliwa kupitia viti maalumu vya wanawake kwa tikiti ya CCM Mkoa wa Singida.

Vivutio vya utalii

[hariri | hariri chanzo]

Yafuatayo ni baadhi tu ya maeneo yenye vivutio vya utalii na utamaduni Wilayani Iramba.

Ziwa Kitangiri na Bonde la Wembere

[hariri | hariri chanzo]

Ziwa hii limepita katika Tarafa za Shelui na Kisiriri wilayani Iramba. Shughuli zifanywazo katika ziwa hili ni uvuvi wa samaki wa aina mbalimbali kama vile: kambare, kamongo, perege, nembe na ningu. Ziwa Kitangiri limekuwa chanzo kikubwa cha uchumi katika wilaya ya Iramba kwa kutoa aina mbalimbali za samaki.

Kuna wanyama waishio humo kama vile kiboko n.k. Pia kuna ndege wengi wa aina mbalimbali wazuri wa kuvutia; ndege hao ni: flamingo, korongo, ndegemwambu (bwana usafi), fongafonga, batamaji, batamzinga n.k.

Aidha pembezoni mwa ziwa hili kuna bonde la mto Wembere.

Nkonta – Ushora – Ndago

[hariri | hariri chanzo]

Kuna mapango ambayo aliishi Gunda Mpwani, mtu aliyekuwa na nguvu za pekee. Pia eneo hilo lina mwamba wenye nyayo za binadamu na wanyama.

Eneo hili lipo kijiji cha Ruruma, Kata ya Kiomboi, Tarafa ya Kisiriri, Hapo kuna nyayo za binadamu na wanyama kama vile mbwa, mbuzi na ng`ombe. Nyayo za binadamu huyo zinajulikana kwa jina la Ntigazi (Mugulu wake Ntegazi).

Kisana Kwa Mang`ombe

[hariri | hariri chanzo]

Eneo hili lipo kijiji cha Kisana, Kata ya Kisiriri, Tarafa ya Kisiriri, kuna michoro ya tembo, ng’ombe na mbuzi kwenye mwamba wa jiwe.

Kisana Wanguu

[hariri | hariri chanzo]

Huko Kisana vilevile kuna eneo la kufanyia matambiko (ibada za asili) kwa Kinyiramba huitwa “kupolya”, eneo la kutambikia huitwa “tyekelo”.

Pango la Kisharita

[hariri | hariri chanzo]

Vilevile kuna pango lenye ngoma zilizotumiwa na watu wa zamani kwa ajili ya matambiko. Ngoma hizo za asili zimehifadhiwa ndani ya pango eneo la Kisana Kisharita, kijiji cha Kisharita, Kata ya Kinampanda, Tarafa ya Kinampanda, ambapo kuna jiwe lililochongwa mithili ya kiti ambacho kilikuwa kinakaliwa na kiongozi wa jadi, Mtemi mdogo Shulua. Alifanya miujiza mingi ya kustaajaabisha kiasi cha kuwafanya adui zake (Wajerumani) kushindwa kumkamata ili wamuue. Mtemi Shulua alijisalimisha kwa Wajerumani na kupelekwa Kilimatinde, Manyoni na hatimaye kunyongwa. Fuvu la Mtemi huyu lipo Ujerumani hadi leo. Jitihada ya kulirudisha Wilayani Iramba bado hazijafanyika.

Nkokilangi

[hariri | hariri chanzo]

Eneo hili lipo kijiji cha Nkokilangi Kata ya Ntwike, Tarafa ya Shelui. Ni maarufu kwa utengenezaji wa chumvi kwa njia ya kienyeji.

Eneo hilo lilitawaliwa na mtemi Kilyoma aliyekuwa na miujiza mbalimbali kama kutoweka mikononi mwa maadui zake bila wao kujua amepotelea wapi. Kilyoma alinyongwa na Wajerumani eneo la Ntwike. Kichwa chake kilipelekwa Ujerumani na hadi leo bado kipo huko.

Ni kijiji maarufu katika historia ya Wilaya ya Iramba, Mkoa wa Singida na Tanzania kwa ujumla, hususani suala la uinjilishaji. Wamisionari kutoka Ujerumani Itanai na Everest walifika Ruruma Desemba 24, 1911 kwa lengo la kujenga kanisa na kueneza Injili. Baadhi ya wazee waliokutana na wamisionari hao ni Lyanga Munkyala, Mkumbo Kilili na Nsimpule Kishei.

Mti wa Kubatizia

[hariri | hariri chanzo]

Huu ni maarufu katika kijiji cha Ruruma, Wilaya ya Iramba Dayosisi ya Kati, kwani mwaka 1914 waumini walibatiziwa mahali hapo kwani hapakuwa na Kanisa miti huo kwa Kinyiramba huitwa “mutuilankolo”. Huo mti ulitumiwa kama eneo la kuabudia waumini wa Ukristo wa Ruruma.

Baadhi ya waumini waliobatizwa ni Yakobo Ntundu, Yesaya Mpondo, Stephano Magia, Mukolamulamu Kidedema na Mathayo Gongia.

Mwaka 1933 waumini wa Kinyiramba walianza kubatizwa kwa majina ya Kikristo lakini yenye asili ya Kinyiramba, kwa mfano majina ya wanaume: Nalompa, Nalogwa, Nagunwa, Napangata, Naukigwa, Nasoloa, Nashokigwa, Nakamia, Nakembetwa, Nalingigwa, Najulwa, Nakomolwa, Nalindilwa, Nalumba, Nalumbikya, Nagomolwa, Naligia, Niitwa, Nasania, Nasagulwa, Napunigwa, Nasunzwa, Nasupya n.k.

Kwa upande wa Wanawake ni: Wansokya, Wasangula, Wankembeta, Wampumbulya, Wanindila, Wantwala, Wanguna, Wanduta, Wamilika, Wankolela, Wankumbasa, Wandegya, Wanonda, Wansugumilya, Wansugamilya, Wandaila, Wanimikya, Wantongela, Wangomola, Wantunguila, Wantungata, Wanzalilya, Wampela, Wamona, Wanduta, Welu, Wampapa, Wandishya, Wampunya, Elinkaila, Eliwaza, Eliwanzita, Winjuka, Wintyapa, Elintongela, Msalawelu, Ulumbi, Lumbikya, Wanumbilya, Ukende, Wanumbikya, Wanansula, Wansola, Tyatawelu, Wingwila, Wampandila, Wanzesya, Wampeta, Wansolania, Wanompela, Wanzita n.k.

Sekenke-Tulya

[hariri | hariri chanzo]

Ndipo ambapo inasadikika kuwepo kwa rasilimali nyingi ikiwemo mafuta na madini ya aina mbalimbali.

Kata za Wilaya ya Iramba - Mkoa wa Singida - Tanzania

Kaselya | Kidaru | Kinampanda | Kiomboi | Kisiriri | Kyengege | Maluga | Mbelekese | Mgongo | Mtekente | Mtoa | Mukulu | Ndago | Ndulungu | Ntwike | Old-Kiomboi | Shelui | Tulya | Ulemo | Urughu


Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Singida bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Iramba kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.