Nenda kwa yaliyomo

Ernst Röhm

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
The printable version is no longer supported and may have rendering errors. Please update your browser bookmarks and please use the default browser print function instead.
Ernst Röhm

Ernst Julius Röhm (München, 28 Novemba 1887 - gerezani, 1 Julai 1934) alikuwa mwanajeshi na mwanasiasa Mjerumani. Alikuwa kati ya wafuasi wa kwanza wa Adolf Hitler na mwanachama muhimu katika chama cha NSDAP aliwa kiongozi wa wanamgambo wa SA. Aliuawa kwa amri ya Hitler.

Mwanajeshi vitani

Röhm alikuwa mwenyeji wa München, mji mkuu wa Bavaria. Akajiunga na jeshi na wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia akapanda ngazi hadi cheo cha kapteni. Baada ya vita aliachishwa kazi kama wanajeshi wengi, akajiunga na kikosi cha wanajeshi wastaafu waliojaribu kuzuia harakati za mapinduzi katika Ujerumani. Aliajiriwa na serikali ya Bavaria kwa huduma ya upelelezi alipotakiwa kutazama vikundi vya kisiasa na kuandaa wanamgambo dhidi ya majaribio ya mapinduzi ya kisoshalisti.

Kukutana na Hitler na kujenga SA

Ernst Röhm na Adolf Hitler

1919 Röhm alikutana na Adolf Hitler akajiunga pamoja naye na chama cha NSDAP akaanzisha kundi la "Sturmabteilung" (SA) kama walinzi wa usalama wa mikutano wa chama na pia kama kundi la kuleta vurugo kwenye mikutano wa vyama vingine. Aliendelea kupanua SA kuwa harakati ya wanamgambo.

Itikadi

Itikadi yake ililenga kwa "mapinduzi ya kizalendo", dhidi ya ubepari na dhidi ya demokrasia. Ilifanana kiasi na itikadi ya ufashisti huko Italia. Itikadi yake ilizaliwa wakati wa vita. Aliona lengo ya maisha katika ushirikiano wa wanaume chini ya viongozi wenye mamlaka. Pesa na biashara hazikuwa na nafasi katika mwelekeo huo. Yale yaliyopatikana yalipaswa kugawiwa kati ya wote jinsi ilivyokuwa vitani. Maadui walipaswa kuvunjwa. Kwa jumla alidharau siasa.

Kutokana na itikadi hii alitofautiana na Hitler aliyepokea pesa kutoka kwa viongozi wa kiuchumi waliotafuta wasaidizi dhidi ya harakati ya kijamaa ya wafanyakazi walioelekea usoshalisti.

Kuachana na Hitler na kurudi

1925 Roehm aliachana na Hitler akajiuzulu na SA akaenda Paraguay kama mshauri wa kijeshi. Lakini 1930 Hitler alimwomba arudi na kuhukua amri ya SA tena.

Kiongozi wa SA tena Roehm aliendelea kuwa na uhusiano mwenye matatatizo na wanasiasa wa NSDAP. Alijisikia mkubwa kwa sababu SA ilikuwa na wanachama wengi kushinda chama chenyewe na vikosi vya SA vilipigana barabarani na wapinzani wa vyama vingine. Aliona ya kwamba jeshi lake la wananchi linapaswa kuchukua nafasi ya jeshi la serikali. Kwa kila namna alijaribu kuongoza SA bila kuathiriwa na maafisa wa NSDAP isipokuwa alimsikia Hitler mwenyewe.

Kusubiri mapinduzi ya kizalendo baada ya 1933

1933 SA ilikuwa na watu 400,000. Baada ya Hitler kuwa mkuu wa serikali tangu 30 Januari 1933 Roehm pamoja na wengine katika SA alitegemea "mapinduzi ya kizalendo". Lakini Hitler alijua ya kwamba mamlaka yake yalitegemea mwanzoni uelewano mzuri na viongozi wa jeshi, wenye mashamba makubwa na mabwana wa viwanda.

Röhm alidai kuunganishwa kwa jeshi la serikali na SA yake akalenga kuwapa wanaSA silaha. Alijaribu pia kudai cheo cha waziri wa jeshi.

1934 Hitler alimwona Röhm na viongozi wa SA kama usumbufu na hatari kwake. Aliandaa pigo dhidi yao. Tar. 30 Juni 1934 viongozi wa SA waliokutana mahali pamoja. Usiku walikamatwa na wanamgambo wa SS kwa amri ya Hitler.

Röhm pamoja na wengine waliuawa gerezani usiku huohuo au siku iliyofuata. Röhm alipewa bastola pamoja na amri ya kujiua. Alipokataa alipigwa risasi.

Serikali ilitangaza baadaye ya kwamba viongozi wa SA waliandaa uasi uliozuiliwa na vyombo vya serikali na chama.