Eritrea
Dola la Eritrea | |
---|---|
ሃገረ ኤርትራ (Kitigrinya) | |
Wimbo wa taifa: ኤርትራ ኤርትራ ኤርትራ (Kitigrinya) "Eritrea, Eritrea, Eritrea" | |
Mahali pa Eritrea | |
Ramani ya Eritrea | |
Mji mkuu na mkubwa nchini | Asmara |
Serikali | Udikteta |
• Rais | Isaias Afwerki |
Eneo | |
• Eneo la jumla | km2 117 600[1] |
Idadi ya watu | |
• Kadirio la 2023 | 6 274 796[1] |
Pato la taifa | Kadirio la 2019 |
• Jumla | USD bilioni 1.98[2] |
• Kwa kila mtu | USD 566[2] |
Pato halisi la taifa | Kadirio la 2019 |
• Jumla | USD bilioni 6.42[2] |
• Kwa kila mtu | USD 1 835[2] |
Maendeleo (2022) | 0.493[3] - duni |
Sarafu | Nakfa |
Majira ya saa | UTC+3 (Afrika Mashariki) |
Msimbo wa simu | +291 |
Msimbo wa ISO 3166 | ER |
Jina la kikoa | .er |
Eritrea ni nchi ya Afrika ya Mashariki. Mashariki na Kusini-Mashariki Eritrea ina pwani ndefu katika Bahari ya Shamu.
Upande wa Magharibi imepakana na Sudan, upande wa Kusini imepakana na Ethiopia, na Kusini-Mashariki kuna nchi ya Djibouti. Eneo hili lote hujulikana pia kama Pembe ya Afrika.
Jina
[hariri | hariri chanzo]Jina la nchi limetungwa mnamo mwaka 1890 na wakoloni wa Italia kutokana na neno la Kigiriki "erythraîa" linalomaanisha “bahari nyekundu” – kwa Kiingereza “Red Sea”. Hii ni kwa sababu Bahari ya Shamu iliitwa "Sinus Erythraeus" na mabaharia Wagiriki au “Mare Erythraeum” kwa Kilatini na Waroma wa kale – maana yake ni "bahari nyekundu".
Jiografia
[hariri | hariri chanzo]Eritrea iko katika eneo la Pembe la Afrika na ina Bahari ya Shamu upande wa kaskazini mashariki. Kwa mchanga wa pwani ulio eneo kame pahali pa kutega samaki ni Funguvisiwa la Dahlak.
Eneo ambalo liko kwa milima kusini si kame vile, lakini hali ya hewa ni poa. Mlima wa juu zaidi ni Soira, ambao uko kati ya nchi, mita 3018 juu ya bahari.
Miji
[hariri | hariri chanzo]Mji mkuu wa Eritrea ni Asmara na miji mingine ni kama vile mji wa bandari Assab kusini mashariki, na pia miji kama Massawa na Keren.
Eneo
[hariri | hariri chanzo]Eritrea imegawiwa katika maeneo 6:
- Kati (Maekel)
- Anseba
- Kisini ziwa lekundu (Debubawi-Keih-Bahri)
- Kaskazini ziwa lekundu (Semienawi-Keih-Bahri)
- Kusini (Debub)
- Gash-Barka
Historia
[hariri | hariri chanzo]Hadi karne ya 19 maeneo ya Eritrea yalikuwa sehemu ya Ethiopia.
Pwani ilikaa karne nyingi chini ya utawala wa Uturuki au baadaye Misri kama nchi zenye nguvu kwenye Bahari ya Shamu.
Historia ya Eritrea kama eneo la pekee jinsi ilivyopata uhuru mwisho wa karne ya 20 ilianza na ukoloni wa Italia.
Mwanzo wa ukoloni wa Italia
[hariri | hariri chanzo]Mnamo Novemba 1869 kampuni ya biashara ya Kiitalia ya Rubattino ilinunua bandari ya Assab kutoka kwa sultani wa Afar. Ilikuwa inatafuta kituo kwa meli zake zilizoanza kupita katika bahari ya Shamu baada ya kufunguliwa kwa Mfereji wa Suez mwaka uleule.
Serikali ya Misri ilipinga mapatano hayo kwa sababu ilidai eneo lilikuwa chini ya amri yake. Makubaliano hayakufikiwa hadi 1882, serikali ya Italia ilipochukua moja kwa moja mali ya kampuni kama koloni lake la kwanza katika Afrika.
Tangu kuporomoka kwa utawala wa Misri nchini Sudan, baada ya vita vya Al-Mahdi, Misri ilijiondoa pia katika pwani ya kusini mwa bahari ya Shamu. Italia ilitumia nafasi hiyo na tarehe 5 Februari 1885 ilipeleka wanajeshi mjini Massawa na kuitangaza kuwa koloni lake.
Waitalia waliendelea kuunganisha maeneo yao ya Assab na Massawa. Baadaye walijaribu kupanua utawala wao kutoka tambarare za pwani hadi nyanda za juu zilizokuwa chini ya Dola la Ethiopia.
Negus Yohanne IV hakufurahia kufika kwa Italia kwa sababu aliamini ya kwamba Massawa iliahidiwa kwake baada ya kuwasaidia Wamisri kujiokoa mbele ya jeshi la Al-Mahdi. Hivyo upanuzi wa Italia katika nyanda za juu ulikutana na upinzani.
Tarehe 26 Januari 1887 jeshi la Waitalia 587 walioelekea kaskazini lilishambuliwa karibu na Massawa kwenye kijiji cha Dogali na kushindwa na Ras Alula aliyekuwa mtemi chini ya Negus ya Ethiopia. Waitalia walipaswa kuongeza wanajeshi 13,000 ili kuhakikisha utawala wao.
Mkataba wa Wuchale na mapigano ya Adowa
[hariri | hariri chanzo]Baada ya Yohanne IV kufariki katika mapigano na jeshi la Al-Mahdi, Waitalia walichukua nafasi hiyo ya kuziingia nyanda za juu za Tigray na kujenga vituo vyao huko.
Mfalme mpya Menelik II tarehe 2 Mei 1889 aliutia sahihi mkataba wa Wuchale uliokubali utawala wa Italia juu ya kanda ya pwani pamoja na maeneo kadhaa ya nyanda za juu za Tigray.
Waitalia walijaribu kumdanganya Negus katika mkataba huo kwa kuingiza maneno katika nakala ya Kiitalia yaliyosema "Ethiopia itakuwa chini ya ulinzi wa Italia". Menelik baada ya kuelewa haya alikana mkataba.
Italia ilijibu kwa kuvamia Ethiopia kwa jeshi kubwa. Jeshi hilo lilishindwa na Waethiopia katika mapigano ya Adowa tarehe 1 Machi 1896. Italia ilipaswa kukubali uhuru wa Ethiopia katika mkataba wa amani tarehe 26 Oktoba 1896. Ethiopia ilikubali mamlaka ya Italia juu ya koloni lake katika kaskazini.
Koloni la Eritrea
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kumaliza mashindano na Ethiopia, Italia tarehe 1 Januari 1890 iliunganisha maeneo yake yote katika koloni lililoitwa Eritrea kufuatana na jina la kale "Bahari ya Eritrea".
Katika kipindi hiki cha utawala wa kikoloni Eritrea ilitokea kama jamii na eneo la pekee. Koloni la Eritrea liliunganisha maeneo matatu yenye tabia za pekee:
- kanda la pwani lililokuwa na historia ndefu ya biashara na mawasiliano na Uarabuni ng'ambo ya Bahari ya Shamu
- kanda la Sahel katika kaskazini-magharibi lililowahi kuwa sehemu ya Sudan
- kanda la nyanda za juu liliwahi kuwa sehemu ya utamaduni wa Watigray Wakristo
Italia ilianzisha miradi ya kufanya Eritrea chanzo cha malighafi kwa ajili ya uchumi wa Italia. Kijiji cha Asmara katika nyanda za juu kilikuwa mji mkuu wa koloni na kupanuliwa kuwa mji kwa ajili ya walowezi Waitalia. Asmara ilipambwa na majengo mazuri ya kisasa.
Katika miaka ya 1930 idadi ya motokaa zilizoendeshwa Asmara ilishinda idadi ya magari ya binafsi mjini Roma. Urithi huo wa majengo umekuwa sababu ya kuingiza Asmara katika orodha ya Urithi wa dunia ya UNESCO.
Waitalia walipanga na kujenga miji mingine kama vitovu vya biashara, mabandari, vituo vya kijeshi au vya kiuchumi.
Idadi ya wakazi wote ilikadiriwa kuwa takriban 200,000 mwaka 1890. Idadi hiyo iliongezeka haraka kufikia zaidi ya 600,000 mnamo 1939. Mabadiliko makubwa yalitokea hasa katika nyanda za juu ambako walowezi Waitalia walianzisha mashamba yao na miji mikubwa zaidi ilijengwa.
Idadi ya wasemaji wa Kitigrinya iliongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 1905 kuwa asilimia 54 mwaka 1939.
Mwisho wa vita kati ya vikundi mbalimbali na kupatikana kwa huduma za kiafya pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula, vyote vilichangia katika kuongezeka kwa idadi ya watu.
Kati ya mabadiliko makubwa ulikuwa ujenzi wa barabara na reli kati ya Massawa, Asmara, Keren na Agordat. Viwanda kadhaa vilianzishwa, pia migodi ya kuchimba mawe au madini.
Sehemu za Waeritrea waliingia katika maisha ya ajira ya kibepari. Hivyo maarifa ya wakazi wa Eritrea hasa katika nyanda za juu yalikuwa tofauti na wenzao katika Ethiopia yenyewe walioendelea kuishi chini ya utaratibu wa kikabaila. Waeritrea walisukumwa katika maisha ya kisasa na uchumi wa fedha.
Hadi mwaka 1940 Eritrea ilikuwa tayari na tabaka la wafanyakazi wa viwandani na katika miji pia tabaka la wasomi wenye elimu ya kisasa.
Baada ya Mussolini kushika serikali, siasa ya Italia ilibadilika. Wafashisti walidharau Waafrika na kuanzisha siasa ya ubaguzi wa rangi. Wenyeji walipewa tu shughuli duni kabisa katika utumishi wa serikali.
Italia ya kifashisti ilifanya mipango ya kulipizia kisasi mapigano ya Adowa ikiandaa vita dhidi ya Ethiopia. Vita vilianza mwaka 1935 kutoka ardhi ya Eritrea. Silaha mpya za Italia (zikiwemo za kikemikali) zilishinda jeshi la Negus, hivyo Ethiopia yote ikawa koloni la Italia kwa miaka michache.
Waitalia walishindwa katika Vita Vikuu vya Pili mwaka 1941, ambapo Waingereza waliteka Ethiopia pamoja na Eritrea.
Baada ya vita vikuu vya pili
[hariri | hariri chanzo]Waingereza walitawala Eritrea hadi 1952.
Mwaka huo Umoja wa Mataifa ulikabidhi Eritrea kwa Ethiopia kama eneo la pekee lenye serikali na bunge lake katika shirikisho.
Mfalme wa Ethiopia, Haile Selassie hakupendezwa na utaratibu huoː alilenga kuunganisha tena Eritrea na Ethiopia na kwa mbinu mbalimbali alipata kura ya bunge la Eritrea ya kujivunja na kuwa jimbo la Ethiopia (1962).
Vita vya kupigania uhuru
[hariri | hariri chanzo]Baada ya tukio hilo vikundi vya wanamgambo walienda porini kupigania kwa silaha uhuru wa Eritrea.
Vita vilitapakaa mwaka 1974 baada ya ufalme kupinduliwa na Umaksi kuingia na rundo la Jeshi lililoitwa Derg kuchukuwa mamlaka, na baadaye kuvamia Eritrea. Ukorofi wa serikali ya Mengistu Haile Mariam ulifanya mengi kuongeza waliotumaini uhuru wa Eritrea katika miaka ya 1980.
Ukombozi wa Eritrea ulitegemea rundo la Eritrean Liberation Front (ELF), ambayo pia inaitwa "Jebha", na Eritrean People's Liberation Front (EPLF), ambaye pia inaitwa "Shaabia". ELF ilikuwa na Waislamu wengi wa pwani na wahifadhi wa tedo za wananchi, na EPLF wengi Wakristo kutoka nyanda za juu za Tigrayi waamini wa Umaksi-Ulenin. ELF ilisaidiwa na wafadhili Waarabu, na EPLF kutoka nchi za kikomunisti zilizokuwa upande wa Urusi, lakini baadaye nchi hizo zikapinduka na kusaidia Derg ya Mengistu Haile Mariam. ELF na EPLF hazikuweza kufanya kazi pamoja na kwa hiyo EPLF ikaimaliza ELF na kuendelea kutafuta uhuru.
Vita vya uhuru vilikwisha mwaka 1991, ambapo Waeritrea na waasi Waethiopia kutoka Tigray walishinda jeshi la Ethiopia na kuteka Addis Ababa; serikali ya Derg ikaanguka miaka miwili baadaye.
Eritrea huru
[hariri | hariri chanzo]Baada ya kura ya wakazi wa Eritrea kukubali karibu kwa kauli moja, uhuru wa nchi ulitangazwa tarehe 24 Mei 1993 na kukubaliwa kimataifa.
Tangu hapo nchi inaendeshwa na chama kimoja bila uchaguzi.
Awali uhusiano na serikali mpya ya Ethiopia ulikuwa mzuri, lakini baada ya miaka ya kwanza ulizorota.
Mwaka 1998 kulitokea vita kati ya Eritrea na Ethiopia vilivyokwisha na ushindi wa Ethiopia. Wanajeshi la kulinda amani la UM wanajaribu kutunza hali ya kutopigana.
Kiongozi wa EPLF, Isaias Afewerki, akawa Rais. Eritrea (EPLF or Shaebia), ikawa chama pekee kinachotawala Eritrea kwa sheria na kubadilisha jina People's Front for Democracy and Justice (PFDJ).
Mwaka 1998, vita vya mpaka na Ethiopia vilileta kifo kwa wanajeshi wengi kwa nchi zote mbili, na Eritrea uchumi wake ukafifia na wananchi wakahangaika sana. Umma wa nchi ukanza kuhama na uchumi kukosa maendeleo. Eritrea ni nchi moja ya Afrika ambapo kuna shida ya mabomu ya ardhi. Serikali ya Ethiopia iliwafukuza WaEritrea ambao waiishi Ethiopia ama watu waliokuwa na utamaduni wa Eritrea baada ya vita na Eritrea. Hii iliwaletea Waeritrea shida na uhamaji.
Hata baada ya kuonyesha maendeleo kidogo kwa uchumi na siasa, serikali ya Eritrea inanyanyasa magazeti na waandishi na pia watu kwa siasa. Serikali yenyewe hata haijaweza kuweka Katiba mpya na kuleta kura ya kidemokrasia.
Baadaye, serikali ya Eritrea imeweza kusisitiza desturi ya ukoloni wa Waitalia ambayo inadai Kanisa na Dini kujiandikisha kwa serikali na kupewa ruhusa wa kuhubiri. Dini zilizopewa ruhusa na serikali ni Kanisa la Kiorthodoksi la Eritrea, Kanisa Katoliki, Kanisa la Mekane Yesus (Walutheri) na Uislamu. Nyingine zote, hasa zenye itikadi kali zimebanwa kote nchini.[4]
Vita vya Eritrea na Ethiopia viliisha mwaka 2000 kwa mashauriano yanayojulikana kama Mapatano ya Algiers. Mojawapo ya makubaliano lilikuwa kuanzisha Muungano wa kimataifa wa kuweka amani, ambao unajulikana kama Muungano wa Kimataifa wa misheni ya Eritrea na Ethiopia (UNMEE); Walinda amani 4,000 wa UM wamebaki kutoka mwezi Agosti 2004.
Makubaliano mengine ya Algiers yalikuwa kuanzisha usawazisho wa mwisho wa mpaka uliyobishaniwa kati ya Eritrea na Ethiopia. Komisheni iliyokuwa na madaraka kutoka kwa UM, iliyoitwa Komisheni ya Mpaka wa Ethiopia na Eritrea (EEBC), baada ya mashauriano mrefu, ilikata maamuzi ya mwisho mnamo Aprili 2002, lakini maamuzi yao yakakataliwa na Ethiopia.
Kutoka Oktoba 2005 bishano la mpaka bado lilibaki kuwa suala nyeti, na wanajeshi wa kulinda amani wa UM walijaribu kutunza hali ya kutopigana.
Hatimaye mwaka 2018 waziri mkuu mpya wa Ethiopia, Abiy Ahmed alimaliza mgogoro huo.
Kumbe mwaka 2020 Eritrea ilimuunga mkono dhidi ya Jimbo la Tigray lililotaka uhuru na kulivamia.
Siasa
[hariri | hariri chanzo]Bunge la Taifa la viti 150, liliyotekezwa mwaka 1993 baada ya Uhuru, lilimchagua Rais wa sasa, Isaias Afewerki. Kura za nchi huwa zinapangwa na kupanguliwa.
Shina za taarifa madaraka za kutangaza habari kwa siasa za nyumbani Eritrea haziko; na Septemba 2001 serikali ilifunga vyombo vya habari vya binafsi, na watu wanaopinga serikali hufungwa bila kushtakiwa. Hii yote ni kutoka taarifa ya washufu wa ulimwengu, kama Waangalizi wa haki za Kibinadamu (Human Rights Watch) na Wakombozi wa Kimataifa (Amnesty International).
Mambo ya nje yanahusu vita na Ethiopia, Sudan na Jibuti. Baada ya wajumbe wa serikali ya Eritrea wa Idara ya mambo ya kigeni kuenda Sudan, ushirikiano umeanza kuwa wa kawaida. Bishano na Ethiopia bado ni wazo kubwa la chuki ambalo limemfanya Rais kuuambia Umoja wa Mataifa ichukue hatua. Uagizaji huu umeelezwa kwa barua kumi na moja za Rais[5].
Watu
[hariri | hariri chanzo]Wakazi wa Eritrea walikadiriwa kuwa 6,380,803 mwaka 2014.
Makabila makubwa ni Watigrinya (55%) na Watigre (30%), ambao wote wawanazungumza lugha za Kiafrika-Kiasia.
Nchi haina lugha rasmi ili kuheshimu sawasawa lugha zote. Hata hivyo Kitigrinya, Kiarabu na Kiingereza vina nafasi za pekee.
Serikali inatambua rasmi Kanisa la Kiorthodoksi la Eritrea, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri pamoja na Uislamu. Makadirio yanatofautiana: Wakristo kwa jumla ni 50-68%, Waislamu 36-48%.
Mwaka 2004 Idara ya taifa ya Marekani (U.S. State Department) iliamua kwamba Eritrea ni Nchi mahsusi ya kufuatiliwa (Country of Particular Concern, au CPC) kwa kufinya uhuru wa dini.
Tazama pia
[hariri | hariri chanzo]- Orodha ya nchi kufuatana na wakazi
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na idadi ya watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na msongamano wa watu
- Orodha ya nchi za Afrika kulingana na pato la taifa
- Demografia ya Afrika
- Orodha ya mito ya Eritrea
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ 1.0 1.1 "Eritrea". The World Factbook (kwa Kiingereza) (tol. la 2025). Shirika la Ujasusi la Marekani. Iliwekwa mnamo 23 Machi 2024.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) (Archived 2023 edition) - ↑ 2.0 2.1 2.2 2.3 "World Economic Outlook Database, October 2023 Edition. (Eritrea)". IMF.org. International Monetary Fund. 10 Oktoba 2023. Iliwekwa mnamo 12 Oktoba 2023.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Human Development Report 2023/2024" (kwa Kiingereza). United Nations Development Programme. 19 Machi 2024. Iliwekwa mnamo 19 Machi 2024.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) - ↑ "Report of the commission of inquiry on human rights in Eritrea". UNHRC website. 2015-06-08. Retrieved 2015-06-09.
- ↑ [1]
Nchi za Afrika | |
---|---|
Afrika ya Kati (Jamhuri ya) | Afrika Kusini | Algeria | Angola | Benin | Botswana | Burkina Faso | Burundi | Cabo Verde | Chad | Cote d'Ivoire | Eritrea | Eswatini | Ethiopia | Gabon | Gambia | Ghana | Guinea | Guinea Bisau | Guinea ya Ikweta | Jibuti | Kamerun | Kenya | Komori | Kongo (Jamhuri ya) | Kongo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya) | Lesotho | Liberia | Libya | Madagaska | Malawi | Mali | Misri | Morisi (Visiwa vya) | Mauritania | Moroko | Msumbiji | Namibia | Niger | Nigeria | Rwanda | Sahara ya Magharibi | Sao Tome na Principe | Senegal | Shelisheli | Sierra Leone | Somalia | Sudan | Sudan Kusini | Tanzania | Togo | Tunisia | Uganda | Zambia | Zimbabwe | |
Maeneo ya Afrika ambayo ni sehemu za nchi nje ya Afrika | |
Hispania: Kanari · Ceuta · Melilla | Italia: Pantelleria · Pelagie | Ufaransa: Mayotte · Réunion | Uingereza: · St. Helena · Diego Garcia | Ureno: Madeira |
Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu. Je unajua kitu kuhusu Eritrea kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni? Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |