ZAIDI YA BILIONI 45 ZALIPA FIDIA KWA WANANCHI WANAOPISHA UHIFADHI SERENGETI

Posted On: Oct, 16 2024
News Images

Wananchi wa Kata ya Nyatwali iliyopo Wilaya ya Bunda Mkoa wa Mara watapisha eneo ambalo ni ushoroba (mapitio) ya wanyama pori wanaopita kwenda kunywa maji Ziwa Victoria wakitokea Hifadhi ya Taifa Serengeti. Eneo hilo ni muhimu kwa ikolojia ya Hifadhi pamoja na shughuli za Uhifadhi na Utalii.

Akiongea na waandishi wa habari Mkuu wa Wilaya ya Bunda Dkt. Vicent Naano Anney amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha kulipa fidia zaidi ya Shilingi Bilioni 45.9 kwa wananchi wanaotakiwa kuhama kupisha ushoroba wa wanyama wanaopita katika eneo hilo hasa Tembo.

Dkt. Anney amesema hayo Wilayani Bunda baada ya kukagua zoezi hilo la ulipaji fidia na kujionea wananchi waliokwisha lipwa fidia wanavyohama. Eneo hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 54.67 na jumla ya mitaa minne ya Tamau, Nyatwali, Kariakoo na Serengeti. Hadi sasa zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi limefikia asilimia 80.6

"Serikali ya awamu ya sita ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshatoa zaidi ya Bilioni 45 kwa ajili ya kulipa fidia kwa wananchi hao ikiwa ni dhamira ya dhati kuhakikisha wananchi hawapati madhara yanayosababishwa na wanyama ikiwemo kujeruhiwa na kuliwa mazoa yao mashambani”

Aidha, Dkt Anney ameeleza kuwa eneo hili la Nyatwali litatumika kwa shughuli za Uhifadhi na Utalii hivyo, litasaidia kukuza Uchumi wa Wilaya ya Bunda kwa kujengwa hoteli na kambi mbalimbali za wageni. Idadi ya Wanyama itaongezeka na wataweza kuonekana kwa uwazi na urahisi wakati wote wakipita kufuata maji ziwa Victoria.

Ameeleza kuwa, wananchi wa Nyatwali wamechukua uamuzi wa kuhama kwa hiyari ili kuepuka madhara na usumbufu wanaoupata wa kuvamiwa mashamba na kuvunjiwa nyumba zao na wanyama hasa Tembo. amewashukuru wananchi waliokwisha anza kuhama na ambao wanaendelea kuhama kwamba itasaidia zoezi hilo kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Serikali itaendelea kuwapa ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu kwa kipindi chote mpaka zoezi litakapokamilika.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi anayeshughulikia masuala ya migogoro ya mipaka TANAPA Mathew Michael Mombo ameeleza kuwa, eneo linalotwaliwa ni kwa ajili ya manufaa muhimu ya ekolojia ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na ni njia ya wanyama kupita (ushoroba) kwenda kufuata maji ziwani.

Ameongeza kuwa “ wananchi wa kata ya Nyatwali wameonyesha mwitikio chanya katika zoezi hilo pamoja na kupongeza kasi ya utekelezaji wake tofauti na maeneo mengine ambapo mazoezi kama hayo yamekuwa yakichukua muda mrefu.

Bw. Ibrahim Shaa, mkazi wa kijiji cha Nyatwali alieleza kuwa “Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mpango wa Serikali yake wa kutuhamisha, hivyo hatuna pingamizi na tayari tushalipokea na mpaka sasa, tayari tumeshalipwa fidia zetu na tupo kwenye maandilizi ya kuondoka kwenye maeneo haya”

Eneo la Nyatwali lipo Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa Serengeti, eneo hili linatarajiwa kuwa na fursa za kitalii ambazo zitanufaisha wananchi wa wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla.