Dola la Roma
Dola la Roma (kwa Kilatini "Imperium Romanum") lilikuwa milki kubwa lililoenea kwa karne kadhaa katika nchi zote zinazopakana na bahari ya Mediteranea (ambayo kwa sababu hiyo iliitwa "Mare Nostrum", yaani "Bahari yetu") na nyinginezo.
Lilianza kwenye mji mkuu wa Roma na rasi ya Italia ikaendelea kuunganisha makabila na mataifa ya nchi nyingi kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia.
Kuanzia karne ya 1 KK Watawala wa Dola wakaitwa makaisari: Kaisari wa kwanza alikuwa Augusto.
Nchi nyingi za sasa ziliwahi kuwa sehemu ya Dola la Roma kama vile Uingereza, Ufaransa, Hispania, Italia, Ugiriki na nchi za Balkani upande wa Ulaya, Moroko, Algeria, Tunisia, Libia na Misri upande wa Afrika, na Uturuki, Syria, Lebanon, Palestina, Jordan na hata Irak upande wa Asia.
Idadi ya wakazi imekadiriwa kuwa ilifikia milioni 50-90, yaani asilimia 20 hivi za watu wote duniani wakati huo.
Lugha ya Dola la Roma ilikuwa Kilatini, ila katika sehemu za mashariki pamoja na Kigiriki cha Kale.
Sehemu ya magharibi ya Dola la Roma iliishia mwaka 476 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Kaisari wa mwisho Romulus Augustulus aliyefukuzwa na jemadari wa Kigermanik wa jeshi la Roma.
Upande wa mashariki Dola la Roma likaendelea hadi mwaka 1453 kwa majina kama "Roma ya Mashariki" au Bizanti.
Dola-mji
haririChanzo cha dola la Roma kilikuwa dola-mji mjini penyewe.
Mji uliundwa katika karne ya 9 KK hivi kwenye vilima kando ya mto Tiber katikati ya rasi ya Italia. Waroma wenyewe walipenda kutaja mwaka 753 KK walioutumia kama chanzo cha kalenda yao "ab Urbe Condita" (a.U.C. = tangu kuundwa kwa Roma). Lakini akiolojia imeonyesha dalili za makazi ya mapema zaidi katika eneo la mji.
Mji ulitawaliwa awali na wafalme. Mwaka 509 KK mfalme wa mwisho alifukuzwa na kipindi cha jamhuri ya Roma kilianza.
Mji wa Roma ulieneza athira yake kwa njia ya mapatano au vita na miji na makabila jirani.
Katiba ya jamhuri
haririKwa karne zilizofuata Waroma walifuata katiba iliyolenga kuzuia asitokee mfalme mpya. Vyeo vyote vilitolewa kwa muda tu kwa njia ya uchaguzi. Madaraka yaligawiwa kati ya ngazi na vyeo mbalimbali. Vyeo vingi vilitolewa kwa watu wawili kwa kipindi kilekile kwa sharti la kwamba hao wapatane na kuangaliana.
- Kila mtu aliruhusiwa kuwa na cheo fulani kwa muda wa mwaka 1 pekee
- Hakuruhusiwa kuwa na kipindi cha pili kwenye cheo kilekile
- Aliyechaguliwa kupata cheo hakuruhusiwa kugombea cheo kingine mara moja
- Kila cheo kilikuwa na nafasi mbili. Hao watendaji wawili waliochanga cheo kimoja walipaswa kupatana; kila mmoja aliweza kufuta maazimio ya mwenzake.
- Mgombea wa cheo fulani alipaswa kutangulia katika utendaji wa cheo cha chini kabla ya kupanda juu
- Kati ya kugombea vyeo viwili mgombea alipaswa kupumzika mwaka mmoja.
Kulikuwa na cheo kimoja pekee kilichotekelezwa na mtu mmoja tu: dikteta. Dikteta aliweza kuchaguliwa katika kipindi cha dharura kama vita kwa muda wa miezi sita. Katika kipindi hiki alifanya maazimio peke yake. Kwa kawaida watendaji wakuu walikuwa makonsuli ("consules") waliochaguliwa kwa muda wa mwaka 1.
Upanuzi katika Italia
haririDola la Roma lilianza kupanuka katika Italia. Mwaka 396 KK mji jirani wa Veio ulitwaliwa na kuharibiwa. Katika karne ya 4 KK vilitokea vita kati ya Roma na majirani na eneo lote la Lazio likatawaliwa na Roma.
Roma ilianzishwa utaratibu wa ushirikiano na majirani. Mara chache tu wapinzani walimalizwa kabisa kama Veio. Mara nyingi walilazimishwa kutia sahihi mikataba ya ushirikiano walimopaswa kuwasaidia Waroma kwa wanajeshi na kutokuwa na uhusiano wowote na makabila ya nje. Makabila na miji iliyoshirikiana vizuri na Roma walipewa uraia wa Roma sawa na wenyeji wa mji wenyewe.
Katika karne ya 3 KK Waroma waliendelea kutwaa sehemu kubwa ya rasi ya Italia. Katika vita dhidi ya Pyrrho wa Epirus (eneo kati ya Albania na Ugiriki wa leo) miaka ya 280 KK - 275 KK Roma ilishinda mara ya kwanza dhidi ya jeshi lililotoka nje ya Italia. Vita hii ilisababisha ubwana wa Roma juu ya miji ya Kigiriki kusini mwa Italia ilipaswa kukubali ubwana wa Roma tangu 275 KK pia makabila ya milimani.
Vita za Wapuni na kipaumbele katika Mediteranea ya magharibi
haririUshindi huo ulisababisha ugomvi na Karthago iliyotawala pwani za Mediteranea pamoja na kisiwa kikubwa cha Sisilia. Hali ya vita ilianza tangu mwaka 264 KK kati ya Roma na watu wa Karthago ("Wafinisia" au "Wapuni" jinsi walivyoitwa na Waroma). Vita hii ya kwanza ilikwisha mwaka 241 KK na Karthago ilipaswa kuwaachia Waroma Sisilia yote. Katika vita hii Waroma waliendelea kushinda baharini pia, si kwenye nchi kavu tu.
Vita ya pili dhidi ya Wapuni (218 KK - 201 KK) ilianzishwa na Karthago. Jemadari Hanibal alitaka kulipiza kisasi akavuka milima ya Alpi kwa tembo zake wa kivita. Alishinda mara kadhaa jeshi la Waroma lakini Waitalia wengine walisimama imara upande wa Roma. Mwishowe Roma ilishinda mara ya pili na Karthago ilipaswa kuwaachia Waroma pwani yote ya kaskazini-magharibi ya Mediteranea pamoja na Gallia (leo Ufaransa) ya kusini, Hispania na visiwa vya Mediteranea. Karthago ilibaki upande wa Afrika tu.
Mabaki ya himaya ya Karthago, pamoja na mji wenyewe, yalimalizwa na Roma katika vita ya tatu dhidi ya Wapuni kati ya miaka 149 KK na 146 KK. Karthago iliharibiwa kabisa na wakazi wote wasiouawa waliuzwa kama watumwa.
Upanuzi katika Ugiriki
haririWakati wa vita ya pili ya Wapuni mfalme Filipo V wa Makedonia aliwahi kuwasaidia Karthago. Roma ilitumia nafasi ya ushindi kupinga upanuzi wa Makedonia katika Ugiriki kwa kusaidia madola madogo za Ugiriki ya kusini dhidi ya Filipo V. Vita hizi kati ya Roma na Makedonia zilikuwa na shabaha za kuzuia kipaumbele cha ufalme wowote wa Ugiriki. Roma likabaki katika siasa ya Ugiriki zaidi kama mtazamaji.
Mwaka 192 KK mfalme Antioko III wa milki ya Waseleuko aliingia kijeshi katika Ugiriki. Roma ikajibu kwa kutuma legioni zake na kuanzisha mfululizo wa vita zilizoendelea hadi mwaka 146 KK. Waseleuko walipaswa kujiondoa kabisa katika Ugiriki. Uwezo wa Makedonia ukapunguzwa na sehemu kubwa ya Ugiriki kuwa majimbo ya Kiroma ya Akaya, Epirus na Makedonia.
Jaribio la mwisho la Wagiriki kutetea mabaki ya uhuru wao lilisababisha uangamizi wa mji wa Korintho mwaka 146 KK pamoja na uharibifu wa Karthago.
Kuingia Asia
haririMwaka 133 KK mfalme wa Pergamon katika Asia Ndogo (Uturuki wa leo) aliyeogopa fitina kati ya warithi wake aliamua kukabidhi milki yake kwa jamhuri ya Roma baada ya kifo chake. Milki hii ikawa jimbo la Kiroma la Asia lililoonekana kuwa jimbo tajiri kabisa. Tukio hili likawa mlango wa Roma kupanua zaidi himaya yake katika mashariki ya Mediteranea.
Jimbo jipya la "Asia" likavuta wanasiasa Waroma wenye hamu ya kujitajirisha likawa kitovu cha ufisadi katika milki ya Roma. Mwanasiasa aliyepata nafasi ya kuwa gavana alikuwa mtu tajiri sana baada ya miaka 2 au 3.
Upanuzi wa Dola la Roma lilileta faida lakini matatizo pia:
- nafasi ya kujitajirisha katika utumishi kwenye majimbo mapya ya nje kulisababisha kuongezeka kwa gharama za kugombea. Maana wanasiasa waliolenga kupata nafasi hizi walikopa na kutumia pesa nyingi ili wapate kura nyingi. Waliamini ya kwamba baada ya ushindi wangeweza kurudisha madeni. Hali hii ilisababisha kuongezeka kwa kiwango cha pesa kilichotumiwa kwa kampeni za uchaguzi kwa jumla.
- baada ya kuingiza maeneo mengi ya mbali Waroma waliona athira za tamaduni za kigeni. Waroma wa miaka ya kwanza ya jamhuri walijivunia maisha bila anasa. Walidharau mapambo na matumizi ya pesa kwa mahitaji ya anasa. Lakini sasa walivuta katika jamii yao watu wa Ugiriki na Asia waliopenda anasa.
Kipindi cha mgogoro
haririMafanikio na upanuzi wa jamhuri ya Kiroma vilileta mabadiliko makubwa. Vilisababisha pia kipindi cha mgogoro kilichoanza kuonekana kwa nguvu pamoja na upanuzi huko Asia.
Tatizo kuu lilikuwa suala la ardhi pamoja na mfumo wa jeshi.
Mfumo wa jeshi ulisimama juu ya msingi wa kila raia kushiriki vitani. Kila raia wa Roma alipaswa kubeba silaha na kujiunga na jeshi kama dola liliamua kuwa vita ni lazima. Kila raia alipaswa kujipatia na kugharimia silaha zake.
Upanuzi wa dola lilileta matatizo. Hasa wakulima wengi wadogo walishuka kiuchumi. Kadiri dola lilivyopanuka na jeshi lilivyopaswa kupiga vita katika maeneo ya mbali, hao wakulima wadogo walipaswa kuondoka kwa muda mrefu zaidi kutoka nyumbani na shambani mwao. Utekelezaji wa kazi ulibaki kwa wazee, wanawake na watoto pekee. Wanaume wenyewe, wenye uwezo wa kazi hasa, waliondoka kwenda vitani na kukaa mbali na kaya kwa vipindi vilivyozidi kuongezeka.
Kinyume chake matajiri hawakupata matatizo hayo. Wakiwa na mashamba makubwa waliweza kununua watumwa wa kutosha walioweza kulima na kutawala mashamba yao pamoja na wazee na wanawake hadi wenyewe waliporudi. Vilevile matajiri walikuwa na uwezo wa kununua silaha bora, pia farasi za kupandia na hivyo kushika vyeo vya juu zaidi jeshini. Vyeo vya juu viliwapa sehemu kubwa zaidi ya mali ya maadui iliyoporwa baada ya ushindi. Kutokana na mapato hayo makubwa zaidi waliweza kununua mashamba makubwa zaidi.
Tokeo lake lilikuwa mabadiliko la kilimo katika Italia: wakulima wadogo walizidi kushuka chini, walipaswa kukopa pesa kwa kujidumu na kuwa na madeni. Mwishowe walipaswa kuuza mashamba yao na kutafuta kazi kama vibarua. Kinyume chake tabaka la wenye mashamba makubwa liliongezewa nguvu na utajiri. Tofauti za kijamii ziliongezeka. Tofauti hizo zilisababisha kutokea kwa kipindi cha machafuko ya kisiasa na ya kijamii ambayo yalipeleka Roma hadi vipindi vya vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Marejeo
hariri- Frank Frost Abbott (1901). A History and Description of Roman Political Institutions. Elibron Classics. ISBN 0-543-92749-0.
- J. A. Crook, Law and Life of Rome, 90 BC–AD 212, 1967 (ISBN 0-8014-9273-4).
- Arther Ferrill, The Fall of the Roman Empire: The Military Explanation, Thames and Hudson, 1988 (ISBN 0-500-27495-9).
- Goldsworthy, Adrian. The Complete Roman Army, Thames and Hudson, 2003 (ISBN 0-500-05124-0).
- Benjamin Isaac, "The Limits of Empire: the Roman Army in the East" Oxford University Press, 1992 (ISBN 0-19-814926-3).
- Andrew Lintott, Imperium Romanum: Politics and administration, 1993 (ISBN 0-415-09375-9).
- Edward Luttwak, The Grand Strategy of the Roman Empire, Johns Hopkins University Press, 1976/1979 (ISBN 0-8018-2158-4).
- Ritti, Tullia; Grewe, Klaus; Kessener, Paul (2007), "A Relief of a Water-powered Stone Saw Mill on a Sarcophagus at Hierapolis and its Implications", Journal of Roman Archaeology, 20: 138–163
- Schnitter, Niklaus (1978), "Römische Talsperren", Antike Welt, 8 (2): 25–32
- Smith, Norman (1970), "The Roman Dams of Subiaco", Technology and Culture, 11 (1): 58–68, doi:10.2307/3102810
- Smith, Norman (1971), A History of Dams, London: Peter Davies, ku. 25–49, ISBN 0-432-15090-0
Marejeo mengine
hariri- John Bagnell Bury, A History of the Roman Empire from its Foundation to the death of Marcus Aurelius, 1913, ISBN 978-1-4367-3416-5
- Duncan B Campbell, The Rise of Imperial Rome, AD 14-193, Osprey, 2013, ISBN 978-1-78096-280-1
- Winston Churchill, A History of the English-Speaking Peoples, Cassell, 1998, ISBN 0-304-34912-7
- Edward Gibbon, The History of the Decline and Fall of the Roman Empire, 1776–1789
- Adrian Goldsworthy. In the Name of Rome: The Men Who Won the Roman Empire, Weidenfield and Nicholson, 2003, ISBN 0-297-84666-3
- Michael Grant, The History of Rome, Faber and Faber, 1993, ISBN 0-571-11461-X
- Antonio Santosuosso, Storming the Heavens: Soldiers, Emperors and Civilians in the Roman Empire, Westview Press, 2001, ISBN 0-8133-3523-X
Viungo vya nje
haririAngalia mengine kuhusu Dola la Roma kwenye miradi mingine ya Wikimedia: | |
Fafanuzi za Kiingereza kutoka Wiktionary | |
picha na media kutoka Commons | |
misaada ya kujisomea kwa Kiingereza kutoka Wikiversity | |
nukuu kutoka Wikiquote | |
matini za ushuhuda na vyanzo kutoka Wikisource | |
vitabu kutoka Wikibooks |
- Romans for Children Ilihifadhiwa 24 Aprili 2009 kwenye Wayback Machine., a BBC website on ancient Rome for children at primary-school level.
- Rome Unleashed Ilihifadhiwa 28 Machi 2014 kwenye Wayback Machine., interactive educational website on ancient Rome for students.
- Interactive map of the Roman Empire at Vici.org Archived 2017-10-10 at Archive-It
- Historical Atlas showing the expansion of the Roman Empire.
- Roman-Empire.net, learning resources and re-enactments.
- The Roman Empire in the First Century (PBS).
- United Nations of Roma Victrix
- The Romans
- The Historical Theater in the Year 400 AD, in Which Both Romans and Barbarians Resided Side by Side in the Eastern Part of the Roman Empire
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Dola la Roma kama enzi zake au matokeo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |